Mauzo ya tiketi za elektroniki kwa mechi tatu kati ya nne za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa keshokutwa (Januari 29 mwaka huu) tayari yameanza, hivyo washabiki na wapenzi wa soka wanatakiwa kununua mapema. Mechi hizo ni kati ya Coastal Union na Yanga itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na ile ya Azam dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Azam Complex. Kwa washabiki wa Dar es Salaam watakaokwenda Tanga kushuhudia mechi kati ya Coastal Union na Yanga wanashauriwa kuanza safari wakiwa na tiketi zao mikononi, hasa kwa wale watakaonunua kupitia maduka ya Fahari Huduma. Tiketi pia zinaweza kununuliwa kupitia mtandao wa M-Pesa kwa kupiga namba *150*03*02#. Kwa wanaotumia CRDB simbanking wanaingia kawaida kwa *150*03. Vilevile tunawakumbusha washabiki kuwa kwa viwanja ambavyo tayari vina mfumo wa tiketi za elektroniki hakuna tiketi zitakazouzwa uwanjani, hivyo wanaokwenda kwenye mechi wanatakiwa kuwa na tiketi zao mikononi.
No comments:
Post a Comment